Lampard aula Championship
Kiungo wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya England Frank Lampard ameteuliwa kuwa meneja mpya wa timu ya ligi ya Championship nchini humo Coventry City kwa mkataba wa miaka miwili na nusu.
Lampard anachukua nafasi ya Mark Robins, ambaye alifutwa kazi mapema mwezi huu. Coventry wako nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Championship baada ya kucheza michezo 17 na hawajashinda katika mechi zao nne zilizopita.
“Nimefurahi kwamba Frank Lampard amekubali kujiunga na klabu yetu kama kocha mkuu. Frank ni mzoefu kwenye michuano ya Ligi na anajua kinachohitajika katika ligi hii ili kufanikiwa,” mmiliki wa klabu hiyo Doug King alisema katika taarifa yake.
Akiwa mchezaji, Lampard aliifungia Chelsea mabao 211 katika mashindano yote ndani ya miaka 13 iliyobeba taji. Awali amewahi kuzinoa Chelsea na Everton kwenye Premier League, na Derby County kwenye Championship.
Lampard atakuwa kwenye benchi la Coventry kwa mara ya kwanza Jumamosi hii dhidi ya Cardiff City katika uwanja wa Coventry Building Society Arena