Nyumbani

Upendo Super Bonanza kufanyika leo

Lengo ni kujenga afya na maadili kwa vijana

DAR ES SALAAM:UMOJA wa Vijana wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mabibo External umewakaribisha vijana wote kushiriki katika Upendo Super Bonanza litakalofanyika leo 2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Makaburi, Mabibo External jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na SpotiLeo, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana KKKT Mabibo External, Erick Kisaule, amesema bonanza hilo linalenga kuwakutanisha vijana katika mazingira ya urafiki, mshikamano na kujenga afya kupitia michezo mbalimbali.

Amesema pamoja na kuimarisha afya za vijana, bonanza hilo ni jukwaa muhimu la kuwasaidia kujiepusha na makundi yenye tabia hatarishi yanayoweza kuathiri maisha yao.

“Mabonanza ya aina hii yanawasaidia vijana kujumuika pamoja, kujenga mahusiano mema na kuachana na tabia zisizofaa kama matumizi ya dawa za kulevya, uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi na mienendo mingine isiyofaa katika jamii,” amesema Kisaule.

Ameongeza kuwa washiriki watapata fursa ya kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, rede, kuvuta kamba, mbio za kukimbia, mbio za ndimu kwenye kijiko pamoja na mchezo wa kukimbiza kuku.

Kwa mujibu wa Kisaule, bonanza hilo linatarajiwa kuanza saa sita mchana hadi jioni na litakuwa wazi kwa vijana wote watakaopenda kushiriki.

Aidha, amesema pamoja na michezo na burudani, kutakuwa na ujumbe wa kiroho wenye lengo la kuwajenga vijana katika maadili mema kwa kuzingatia neno la Mungu.

“Neno la mwaka katika bonanza hili ni, ‘Jinsi gani kijana ajisafishe njia yake? Kwa kutii na kulifuata neno la Mungu.’ Hivyo tunawakaribisha vijana wote kujitokeza kwa wingi kushiriki siku hiyo muhimu,” amesema.

Miongoni mwa shirika zitakazoshiriki Upendo Super Bonanza ni pamoja na Mabibo External wenyeji, Changanyikeni, Mtaa wa Kisiwani na Miongo la ndege,

Related Articles

Back to top button