EPL

Andoni Iraola kutua Anfield: Enzi mpya Kuanza Liverpool

UINGEREZA: MABINGWA wa soka la England mara 20, Liverpool F.C., wapo kwenye hatua za mwisho za kufungua ukurasa mpya baada ya kufikia makubaliano ya kumteua Andoni Iraola kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili utakaodumu hadi Juni 2028.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na mwandishi wa masuala ya soka duniani Fabrizio Romano, kila kitu kimekamilika mezani na sasa kilichobaki ni kutangazwa rasmi kwa kocha huyo wa Hispania, jambo linalotarajiwa kufanyika ndani ya siku chache zijazo.

Ujio wa Iraola unaonekana kuwa mwanzo wa zama mpya ndani ya viunga vya Anfield, huku akitarajiwa kurithi mikoba ya Arne Slot ambaye amekuwa akiiongoza Liverpool katika kipindi cha hivi karibuni.

Kocha huyo anayesifika kwa soka la kasi, presha ya juu uwanjani na falsafa ya kushambulia bila woga, anatajwa kuwa tayari ameshaweka ramani ya kikosi chake cha ufundi kitakachotumika hapo Anfield.

Taarifa zinaeleza kuwa Iraola anataka kuingia Anfield akiwa sambamba na watu wake wa karibu anaowaamini katika safari yake ya ukocha, akiwemo Pablo de la Torre, Tommy Elphick, Shaun Cooper pamoja na Tom Webber.

Mashabiki wa Liverpool sasa wanasubiri kwa hamu kuona namna mbunifu huyo wa Hispania atakavyolibadilisha jahazi la The Reds na kulirejesha katika makali yake ya kutikisa England na Ulaya.

Liverpool F.C. ni mabingwa wa soka la England mara 20, idadi inayowafanya kuwa miongoni mwa vilabu vyenye mataji mengi zaidi ya ligi kuu ya England. Taji lao la karibuni lilipatikana msimu wa 2024/25 chini ya kocha Arne Slot.

Related Articles

Back to top button