Venus Williams ‘apigwa’ na kinda

MIAMI: GWIJI wa mchezo wa tenisi Venus Williams ameshindwa kuonesha umwamba wake katika mchezo huo baada ya kushindwa vibaya na mchezaji chipukizi Francesca Jones katika mashindano ya Miami Open yaliyofanyika nchini Marekani usiku wa kuamkia leo Machi 20.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, Francesca Jones aliibuka na ushindi wa seti mbili mfululizo kwa alama 7-5, 7-5, akionesha kiwango cha juu dhidi ya mkongwe huyo aliyewahi kuwa namba moja duniani katika mchezo huo.
Ushindi huo unaelezwa kuwa wa kihistoria kwa Jones, ambaye aliwahi kumtaja Venus Williams kama mtu wake wa mfano (idol) tangu akiwa mdogo.
Kwa upande wake, Venus Williams alionesha mapambano makali ndani ya uwanja, lakini alishindwa kuhimili kasi na nguvu ya mpinzani wake huyo chipukizi.
Matokeo hayo yanaendelea kuonesha ushindani mkubwa uliopo kwa sasa katika tenisi ya wanawake, huku kizazi kipya cha wachezaji kikizidi kujitokeza na kuleta changamoto kwa mastaa waliotengeneza historia kubwa kwenye mchezo huo.
Kwa ushindi huo, Francesca Jones anaendelea kujijengea jina katika ramani ya tenisi duniani, huku Venus Williams akibaki kuwa mmoja wa wachezaji wenye heshima kubwa licha ya matokeo hayo mabovu.




