Wavu Dar kufanyika Februari 28
DAR ES SALAAM: TIMU 20 za Seria A na B kwa wanawake na wanaume zinatarajia kushiriki Ligi ya Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es Salaam itakayoanza kutimua vumbi Februari 28 mwaka huu katika viwanja vya Kampala International University Tanzania (KIUT).
Katibu wa Chama cha Wavu Dar es Salaam DAREVA, Clement Athanas, amesema kuwa kati ya timu hizo, 18 zinatoka mkoani Dar es Salaam huku mbili zikitoka mkoa wa Pwani, jambo linalotarajiwa kuongeza ushindani na hamasa kwa wapenzi wa mchezo huo.
Amesema timu zote zinatakiwa kuthibitisha ushiriki wao kwa kulipa ada ya usajili kwa wakati ili kuipa kamati ya maandalizi nafasi ya kukamilisha taratibu zote mapema.
“Msimu huu ligi itachezwa kwa mtindo maalum ambapo timu zote za Seria A na B zitacheza ligi moja kwa pamoja katika hatua za awali. Hata hivyo, zitakapofika hatua ya mtoano (play-off), kila kundi litacheza kivyake, yaani Seria A upande wake na Seria B upande wake,” amesema.
Ameeleza lengo la mfumo huo ni kuwapa wachezaji nafasi kubwa ya kucheza mechi nyingi zaidi, kukuza vipaji na kuongeza ushindani miongoni mwa klabu.
Amesema maandalizi ya ligi hiyo yamekamilika, huku akieleza kuwa mashabiki wanatarajia kushuhudia msimu wenye ushindani mkubwa zaidi kutokana na klabu nyingi kufanya usajili wa wachezaji wapya ili kujiimarisha.
“Sio Dar es Salaam tu, bali wapenzi na mashabiki wote wa mpira wa wavu nchini wanatarajia kushuhudia ligi bora zaidi mwaka huu. Tunawaalika wote kufika katika viwanja vya KIUT Februari 28 kushuhudia uzinduzi rasmi wa ligi,” amesema.



