KIUT Wavu yafungiwa kwa utovu wa nidhamu

DAR ES SALAAM: Chama cha Mpira wa Wavu Dar es Salaam (Dareva) kimeifungia mwaka mmoja Kampala International University (KIUT) kutojihusisha na mchezo huo kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Dareva Fred Mshangama, timu ya wanaume ya Wavu ilionesha utovu wa nidhamu wakati wa sherehe za ufungaji wa Ligi hiyo hivi karibuni.
“Adhabu itahusisha benchi la ufundi, wachezaji na itadumu kwa miezi 12 kuanzia Julai mwaka huu hadi Julai mwakani, tunazihimiza timu kuwa makini na kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa,”amesema Mshangama.
Katibu Mkuu wa Dareva Yusufu Mkarambati alitolea ufafanuzi suala hilo na kuiambia Dailynews Digital Leo kuwa KIUT walifanya fujo kwenye fainali dhidi ya Jeshi Stars Ligi Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kushindwa kwa pointi 3-2.
“Baada ya kufungwa na Jeshi Stars walilalamika kuwa wameonewa na mwamuzi hata mchezo ulipoisha waligoma kuchukua zawadi za mshindi wa pili wakaanza kutoa maneno makali ya matusi na lawama kwa viongozi, na baadaye kuzima taa”amesema.
Amesema licha ya kufungiwa uongozi wa KIUT hawajajitokeza kuomba msamaha ila baadhi ya wachezaji ndo walioomba msamaha.
Kufungiwa huko kuliathiri pia, ushiriki wao kwenye ligi ya taifa hali iliyopelekea kuondolewa kwenye mashindano mwezi uliopita.
Washiriki wanne waliofanya vizuri ligi mkoa wa Dar es Salaam walitakiwa kushiriki kwenye ligi ya taifa lakini baada ya kupewa barua ya kufungiwa waliondolewa mashindanoni.