Nyavu

JKT wanawake mambo safi DAREVA

DAR ES SALAAM: LIGI ya Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es Salaam (DAREVA) imeendelea kushika kasi huku ushindani ukizidi kupamba moto, katika michezo inayoendelea kupigwa kwenye Uwanja wa KIUT, jijini Dar es Salaam.

Katika michezo ya jana, timu ya JKT imeendelea kuonesha ubora wake baada ya kuibuka na ushindi wa seti 3-0 dhidi ya Chui, matokeo yaliyoendeleza mwenendo wake mzuri kwenye ligi hiyo.

Mbali na ushindi huo, JKT wanaume pia iliendeleza ubabe wake kwa kuichapa Best Six kwa seti 3-0, na hivyo kuonesha wazi dhamira yao ya kuwania mafanikio makubwa msimu huu.

Kutokana na ushindi huo, JKT wanawake imeendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 14, na wanaume nafasi ya nne kwa pointi 14 hali inayoiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuwania ubingwa huku ligi ikiendelea kushika kasi kadri inavyosonga mbele.

Ushindani katika Ligi ya wanaume ni mkubwa, huku High Voltage ikiwa na michezo saba ikijikusanyia pointi 19, ikifuatiwa na Jeshi Stars aliyecheza michezo sita na pointi 18, huku Nyika ikimalizia nafasi ya tatu kwa kucheza michezo saba na pointi 14. JKT Wanaume wanashika nafasi ya nne kwa pointi 14, huku Best Six ikiwa ya tano kwa pointi 11.
Mechi za wanawake
Kwa upande wa wanawake, JKT ikiwa imecheza michezo saba imeshikilia nafasi ya kwanza kwa pointi 14, ikifuatiwa na KIUT, aliyecheza michezo mitano na pointi 13, huku nafasi ya tatu ikienda kwa Chui, aliyecheza michezo mitano na pointi 12.

Matokeo hayo yanaashiria wazi kuwa ushindani wa DAREVA msimu huu ni mkubwa, huku timu mbalimbali zikijipanga kuhakikisha zinamaliza katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Related Articles

Back to top button