Ligi Daraja La Kwanza

Yanga yanasa mrithi wa Lomalisa

DAR ES SALAAM: BAADA ya kupata mafanikio kwa mabeki kadhaa kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) timu ya Yanga imeendelea kuelekeza ndoano yake katika nchi hiyo ambapo kwa sasa imenasa saini ya beki wa kushoto Shadrack Issaka Boka kutoka Klabu ya Saint Eloi Lupopo.

Beki huyo wa kushoto mwenye miaka 25 ameingia makubalino ya mkataba wa awali wa miaka miwili kuitumikia klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1935 yenye maskani yake Jangwani Jijini Dar es Salaam.

Boka anatarajiwa kuchukua nafasi ya beki mwenzake Joyce Lomalisa ambaye Yanga haijaonyesha nia ya kuendelea naye.

Taarifa kutoka vyanzo vya ndani ya timu hiyo vimeiambia SpotiLeo kwamba Rais wa timu hiyo, Hersi Said amefanya mazungumzo na FC Lupopo tangu mwezi Mei mwaka jana wakati alipokwenda nchini humo kwa mwaliko wa Rais wa TP Mazembe Moise Katumbi kisha akashuhudia mechi ya Saint Eloi Lupopo na Maniema Union zilizotoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1.

Hersi alitumia fursa hiyo kukamilisha kunasa saini ya Boka aliyejiunga na miamba hiyo ya Congo, FC Lupopo mwaka 2021 na kinachosubiriwa sasa ni mchezaji huyo atue nchini kuungana na wenzake wanaotarajiwa kuanza kambi mapema mwezi ujao.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema timu yao imeshafanya usajili kwa baadhi ya wachezaji na kwa sasa kazi iliyobaki ni kupata barua kutoka klabu walizomalizana nao pia kutambulisha wachezaji wapya.

“Tumefanya usajili mkubwa utaleta mafanikio makubwa katika klabu yetu, tumegusa nafasi zote kulingana na mapendekezo ya Kocha Gamondi, tumesajili wachezaji watakaotupa ushindani ndani ya Yanga ili kucheza fainali ya Afrika,” ameeleza Kamwe.

Boka anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na Yanga baada ya kukamilika kwa usajili wa Prince Dube anayeaminika kusaini miaka miwili wa kutumia Yanga baada ya kuvunja mkataba na Azam FC ya Chamazi jijini Dar es Salaam.

Related Articles

Back to top button