BAADA ya mtani wake wa jadi, Simba kudondosha alama kwa kutoka sare ya goli 1-1 na Azam katika mchezo wa Ligi kuu Tanzania Bara, Yanga leo inashuka dimbani kukabili KMC.
Vinara hao wa ligi wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuipa kichapo cha magoli 3-1 TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika mchezo wa Kombe la shirikisho Afrika hatua ya makundi uliopigwa Februari 19, Dar es Salaam.
Iwapo Yanga inayoongoza ligi hiyo itashinda katika mchezo huo utakaofanyika uwanja wa Benjamin Mkapa itafikisha alama 62 na kuiacha Simba iliyopo nafasi ya pili kwa tofauti ya alama 8.
KMC inashika nafasi ya 12 ikiwa na alama 23 baada ya michezo 22.
Katika mchezo wa dabi ya Mzizima, Azam ndio ilikuwa ya kwanza kupata goli la kushtukiza dakika 1 ya mchezo likifungwa na Prince Dube kabla ya Simba kusawazisha kwa goli la kujifunga la Abdallah Kheri wa Azam dakika 90.