Straika la magoli Simba, latangaza vita Ligi kuu
DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa Simba, Lionel Ateba ni kama ametuma salama kwa makipa wa timu pinzani kwa kutamka wazi kuwa atafunga sana na kusaidia timu yake kufikia malengo kwa msimu wa 2024/25.
Ateba alianza kuonyesha makeke yake mchezo wa kirafiki wa Kimataifa dhidi ya Al Hilal ya Sudan uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita dimba la KMC Complex Mwenge jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1, Ateba ndiye aliyewatanguliza Wekundu hao wa Msimbazi, kwa shuti kali kwa guu la kushoto akiunganisha krosi iliyochongwa na Ladack Chasambi kabla ya wageni kusawazisha.
Mshambuliaji huyo, amesema tofauti na watu wengi nchini wanavyomfikiria, kwake kufunga mabao ni jamb0 ambalo amelizoea, hivyo alishangaa kuona baadhi ya mashabiki wakiwa na wasiwasi naye.
Amesema kutokana na upendo na ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzake, wakiwa nje na ndani ya uwanja, anaona atapachika mabao mengi na kuvunja rekodi alizoziweka Ligi mbalimbali alizopita lengo likiwa ni kuipeleka mbali timu hiyo.
“Nimeanza soka langu Tanzania kwa amani na furaha, mechi ya kwanza tu kucheza nimefunga, tena nimefunga dhidi ya timu kubwa, timu ngumu, Al Hilal, nitaendelea kufanya mazoezi kwa bidii, nitaendelea kujituma ili kuweza kushinda mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya AI Ahly Tripoli.
“Naamini kwenye mchezo huo nitakuwa vizuri zaidi na tutafanya vema. Malengo ya Simba ni kutwaa makombe msimu huu ndio maana nimesema nitashirikiana na wenzangu kuhakikisha tunapata kile tunachokihitaji” amesema straika huyo aliyesajiliwa kama mbadala wa Freddy Michael.