Wolper na Rich Mitindo wamaliza tofauti, mambo safi

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu nchini, Jacqueline Wolper, ameweka bayana kuwa amemaliza tofauti zake na mume wake, Richard maarufu kama Rich Mitindo, baada ya kumuomba radhi kwa makosa yaliyopita.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Wolper ameweka picha na video, akieleza kuwa licha ya changamoto walizopitia, anaamini kuwa Mungu alipanga wao wawe mwili mmoja.
“Najua mambo mengi yametokea, lakini kubwa zaidi ni kwamba wewe ni baba wa wanangu, na wanakuona kama shujaa wao. Maisha lazima yaendelee, mume wangu, nisamehe pale ninapokosea na kufanya maamuzi kwa hasira. Lakini pia nimekusamehe kwa kila kitu. Najua moyo wako na natambua kuwa bond yetu ni ya kipekee. Jinsi tunavyoelewana ndilo jambo la muhimu kwangu. Nashukuru kwa kuwa wewe ni mume wangu, na naamini Mungu alikuwa na sababu zake alipopanga mimi na wewe tuwe mwili mmoja.Niseme wazi kuwa nimekusamehe, Baba P, kwa yote yaliyopita. Pia, namuomba Mungu asituache, kwani bila yeye hatuwezi kufanya lolote” ameandika Wolper.
Kwa upande wake, Rich Mitindo naye amejibu kwa maneno yenye hisia kali, akikiri kuwa hakuna uhusiano usio na changamoto, lakini wao wana nia ya kuendelea pamoja.
“Mke wangu, najua nina dosari zangu. Nafanya makosa na wakati mwingine navuka mipaka. Nakiri kuwa kuumizana na kubishana kunaweza kukatisha tamaa na kuathiri mahusiano yetu.Lakini sikukatii tamaa. Ikiwa nia zetu zinalingana, kwanini tuendelee kupingana na kuona mapenzi mabaya? Naomba tuache yaliyopita na tuangalie maisha yajayo yaliyojaa upendo mwingi.Nakupenda zaidi ya maneno yenyewe. Nakukumbusha kuwa muda mwingine najitahidi kuwa bora kwako, lakini mimi ni binadamu, sijakamilika. Nisamehe ninapoteleza. Ninapokosea, unaweza kuhisi kama sikupendi, lakini niamini, nakupenda zaidi ya unavyofikiria. I love you, mke wangu”, ameandika Rich Mitindo.