Ligi Kuu

Wanachama Yanga watulizwa, Mzee Magoma kazi anayo!

DAR ES SALAAM: MKURUGENZI wa Sheria wa timu ya Yanga, Simon Patrick amesema wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwapa muda na kupitia shauri la madai yanayolikabili Baraza la Wadhamini na uongozi wa klabu hiyo kwakuwa ni batili kikatiba.

Mwanasheria huyo amesema Novemba 2022, Juma Ally na Geofrey Mwaipopo, walifungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, msingi wa madai yao ni kuwa hawalitambui Baraza la Wadhamini la Yanga kutokana na kutoitambua Katiba ya 2010 ambayo haijasajiliwa na RITA, wanadai wanachama wote sio halali hivyo viongozi wote na Wanachama wote ambao waliingia kwa mujibu wa katiba hiyo ni batili.

Akizungumza hayo katika makao makuu ya klabu ya Yanga, Simon amesema Juni 16, mwaka huu uongozi ulipokea taarifa kutoka mahakamani na kufanya uchunguzi na kugundua mambo mbalimbali.

Amesema baada ya wanasheria wa Yanga kufanya uchunguzi, wamegundua kuwa walalamikaji Juma na Mwaipopo waliofungua kesi wakitaka Rais wa Yanga, Hersi Said na viongozi wengine waachie ngazi, walighushi sahihi ya klabu na baraza la wadhamini inayoundwa na Mama Fatma Karume pamoja na Jabir Katundu na kushinikiza Mahakama iwape ushindi na iridhie wapewe timu na mali zote za klabu waendeshe wao.

“Watu hawa Juma Ally na Geofrey Mwaipopo waliojiita wanachama wa Yanga, wameitaka mahakama ituondoe katika Uongozi, pia walikuwa wanataka kazi zote zilizofanywa na viongozi hawa zitambuliwe kama batili na waletewe mapato na matumizi yote.

Kesi ilianza kusikilizwa na mlalamikiwa namba moja ni Yanga, akifuatia Mama Karume, Mzee Katundu na Abeid Mohamed aliwasilisha ushahidi au utetezi ambao ulisainiwa na klabu, akidai wote wamemteua kuwawakilisha katika mwenendo wa kesi hiyo, na Abeid alikuwa anakubali kila kitu kinacholalamikiwa akidai anawawakilisha wengine na ikasababisha Mahakama kuwapa ushindi walalamikaji,” amesema na kuongeza

Mei mwaka huu, walalamikaji hao walipeleka maombi yao mbele ya Hakimu Mkazi Kisutu wakiomba Mahakama iwasaidie kulitoa na kulifuta Baraza zima la Wadhamani wa Yanga na kuutoa uongozi wote wa klabu na kutaka wakabidhiwe timu na ‘assets‘ zote za klabu waendeshe wao,” amesema Simon.

Amesema baada ya wanasheria wa Yanga kufuatilia kiundani wakabaini wameghushi saini na pia walalamikaji hao sio wanachama wa Yanga, hivyo klabu hiyo itaiomba mahakama kuongeza muda wa kupitia shauri na kukata rufaa dhidi ya hukumu kwa kuwa muda wa kukata rufaa umeshapita.

Amewataka wanachama wa klabu hiyo kongwe nchini kuwa watulivu kwani jambo hilo lipo kwenye mikono salama na wanaamini haki itatendeka.

Related Articles

Back to top button