Nyumbani

Mchungahela ateuliwa kuongoza kamati ya uchaguzi Yanga

DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga imetangaza uteuzi wa wajumbe watano watakaounda Kamati ya Uchaguzi baada ya kupitishwa na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo huku wakili Malangwe Mchungahela akiteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 12, 2026 na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, wajumbe walioteuliwa ni wakili Samuel Mangesho, Godfrey Mapunda, Nelson Mwakingwe pamoja na Yassir Nassor.

Katika uteuzi huo, wakili Malangwe Mchungahela amepewa jukumu la Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi huku wakili Samuel Mangesho akiteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa uteuzi huo umefanywa na Kamati ya Utendaji ya klabu kwa lengo la kusimamia mchakato wa uchaguzi wa Yanga kwa mujibu wa taratibu na kanuni za klabu.

Hatua hiyo inafungua rasmi maandalizi ya mchakato wa uchaguzi ndani ya klabu hiyo yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam, huku wanachama, wapenzi na mashabiki wakisubiri hatua nyingine zitakazofuata kuhusu ratiba ya uchaguzi huo.

Mchungahela aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) miaka ya hivi karibuni.

Related Articles

Back to top button