Melis Medo hakuna kulala Kagera Sugar

KOCHA Mkuu mpya wa Kagera Sugar Melis Medo tayari ameanza kibarua cha kukinoa kikosi cha wanankurukumbi.
Medo amejiunga na Kagera akitokea Mtibwa Sugar na leo ametambulishwa kunako klabu ya Kagera Sugar huku akioneshwa kuanza kazi ya kuifundisha timu hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Klabu wa Kagera Thabit Kandoro amemkabidhi jezi Kocha huyo kama ishara ya kumkaribisha katika familia hiyo.
“Karibu kwenye familia ya Kagera Sugar Melis Medo, timu bora ukanda wa ziwa,”ilisema taarifa yao.
Kocha huyo kibarua chake cha kwanza ni mchezo dhidi ya Pamba Jiji utakaochezwa Jumapili ya wiki hii kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Medo anachukua nafasi ya Paul Nkata aliyevunjiwa mkataba na klabu hiyo baada ya uongozi kushindwa kuridhishwa na mwenendo wa matokeo ya mechi za Ligi Kuu.
Katika michezo saba, Kagera ilishinda mmoja, sare moja na kupoteza mitano hivyo, ujio wa Medo unatarajiwa kuleta matumaini mapya ndani ya klabu hiyo.