Yanga yatoa siku 13 matawi yafanye uchaguzi

DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga, Wakili Malangwe Mchungahela, ametangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo kwa kuyaagiza matawi yote yenye sifa kufanya uchaguzi wa viongozi na wajumbe kuanzia Juni 13 hadi Juni 26, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mchungahela amesema hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa klabu kufuatia muda wa uongozi wa sasa kwenda kumalizika Julai mwaka huu kwa mujibu wa Ibara ya 29 ya Katiba ya Yanga inayotaja kuwa Kamati ya Utendaji hutumikia kwa kipindi cha miaka minne.
Amesema uchaguzi mkuu uliopita ulifanyika mwaka 2022, hivyo kipindi cha uongozi wa sasa kinafikia tamati na ni lazima taratibu zote za uchaguzi zifuatwe kwa mujibu wa katiba.
“Tunatoa maagizo kwa matawi ya Yanga kufanya uchaguzi kuanzia kesho tarehe 13 Juni 2026 mpaka tarehe 26 Juni 2026. Wakikamilisha uchaguzi huo wanapaswa kuleta majina hayo hapa klabuni kwa lengo la kuendelea na taratibu za uchaguzi mkuu wa klabu. Uchaguzi huo unapaswa kufuata Katiba ya Klabu,” amesema Mchungahela.
Alifafanua kuwa wajumbe watakaoshiriki mkutano mkuu wa uchaguzi watatokana na matawi yaliyokidhi vigezo vya kikatiba, ambapo kila tawi litatoa wajumbe watano ambao ni Mwenyekiti, Katibu, Mweka Hazina pamoja na wajumbe wawili wa mkutano mkuu, mmoja akiwa mwanamke endapo atapatikana.
Mchungahela amesisitiza kuwa matawi yote yanapaswa kuhuisha au kuunda kamati za uchaguzi mara moja ili kuhakikisha mchakato huo unafanyika ndani ya muda uliopangwa.
Aidha, ameongeza kuwa matawi yatakayoruhusiwa kushiriki katika uchaguzi mkuu ni yale yenye wanachama wasiopungua 100 na wasiozidi 500 kwa matawi ya ndani ya nchi, huku matawi ya nje ya Tanzania yakitakiwa kuwa na angalau wanachama 20.
Mchungahela amesema kuwa baada ya kupokea majina ya wajumbe kutoka matawini, Kamati ya Uchaguzi itatangaza hatua zinazofuata kuelekea mkutano mkuu na uchaguzi wa viongozi wa Yanga kwa kipindi kijacho.




