Azam FC haifungiki kiurahisi

MANYARA: TIMU ya Azam FC imeendelea kuonesha sura mbili tofauti ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Mbeya City katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara jana.
Matokeo hayo yanaifanya Azam kufikisha jumla ya sare 10 katika michezo 18 ya ligi msimu huu, ikiwa ndiyo timu inayoongoza kwa idadi kubwa ya sare, hali inayoibua maswali juu ya uwezo wao wa kubadilisha matokeo kuwa ushindi.
Pamoja na wingi wa sare hizo, takwimu zinaonesha Azam imekuwa na mwendo usioridhisha katika michezo ya karibuni, ikishinda mchezo mmoja pekee kati ya mitano iliyopita, jambo linaloathiri kasi yao ya kuwania nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.
Hata hivyo, pamoja na changamoto ya kupata ushindi, Azam inaendelea kujivunia uimara wa safu yake ya ulinzi.
Timu hiyo ni miongoni mwa timu chache ambazo bado hazijapoteza mchezo wowote msimu huu, sambamba na Yanga.
Katika upande wa ulinzi, Azam pia imeonesha kiwango cha juu kwa kuruhusu mabao machache, ikiwa imefungwa mabao matano pekee hadi sasa. Takwimu hizo zinawafanya kuwa miongoni mwa timu zenye safu imara zaidi ya ulinzi, zikifuatia Yanga waliofungwa mabao matatu na Simba wenye mabao sita.
Pamoja na uimara huo, wachambuzi wa soka wanaona Azam inahitaji kuongeza makali katika safu ya ushambuliaji ili iweze kubadilisha sare hizo nyingi kuwa ushindi, hatua itakayowaweka katika nafasi nzuri zaidi ya ushindani wa ubingwa.




