Bidhaa za urembo kuongezewa Ushuru hadi Asilimia 15

DODOMA: WAZIRI wa Fedha, Khamis Mussa Omar, amesema Serikali imependekeza kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwa mashine za kukaushia rangi za kucha za UV/LED zinazoingizwa nchini na kutambulika kwa HS Code 8516.79.00.
Akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri Khamis amesema hatua hiyo inalenga kupunguza athari za kiafya zinazoweza kusababishwa na matumizi ya mashine hizo, ikiwemo hatari ya ugonjwa wa saratani, pamoja na kuongeza wigo wa kodi nchini.
Amesema utekelezaji wa pendekezo hilo unatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha sh. milioni 566.5.
Katika hatua nyingine, Serikali imependekeza kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwa bidhaa za urembo zinazoingizwa nchini kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15. Bidhaa hizo zinatambulika chini ya HS Heading 33.03, 33.04, 33.05 na 33.07.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, lengo la ongezeko hilo ni kuongeza mapato ya Serikali na kuoanisha viwango vya ushuru vinavyotozwa nchini na vile vinavyotumika katika baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zikiwemo Kenya, Uganda na Rwanda.




