Moallin: Kila mechi ni fainali katika mbio za ubingwa

KIGOMA: KOCHA Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Mashujaa FC utakaochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, akisisitiza kuwa kila mechi iliyosalia ni fainali katika harakati za kutwaa ubingwa wa tano mfululizo.
Moallin amesema maandalizi ya timu yamekwenda vizuri wakati wa dirisha la mapumziko ya FIFA na wachezaji wake wana hamasa kubwa ya kurejea kwenye mechi za Ligi Kuu ya NBC.
“Kwanza kabisa, maandalizi yanaendelea vizuri kuelekea mchezo wa kesho. Tulikuwa na kipindi kizuri cha mapumziko ambapo tulipata muda mzuri wa maandalizi. Ninafurahi kuona wachezaji wangu wana hamasa kubwa na wako tayari kurejea kwenye mechi za mwisho za ligi,” amesema.
Kocha huyo amesema wanaiheshimu Mashujaa FC kama wanavyoheshimu timu zote lakini wamefika Kigoma kwa lengo moja la kusaka ushindi.
“Hakuna mchezo rahisi katika ligi hii. Haijalishi tunacheza na timu ya mwisho kwenye msimamo au timu ya pili, kila mchezo kwetu ni fainali. Lengo letu ni kutwaa ubingwa wa tano na kila mchezo ni hatua muhimu kuelekea kufanikisha azma hiyo,” amesema.
Aidha, aliwapongeza wachezaji wake kwa kuendelea kuwa na nidhamu na kujituma licha ya presha ya mbio za ubingwa, huku akiwashukuru mashabiki wa Kigoma kwa mapokezi makubwa waliyoipa timu hiyo.

Golikipa wa Yanga Hussein Masalanga amesema “Tangu tulipowasili tumepokea mapokezi mazuri sana kutoka kwa mashabiki wetu wa Kigoma. Walikuja kwa wingi kutupokea na hata walihudhuria mazoezi yetu ya jana. Tunafurahi sana kuwaona na tunataka kuwapa burudani nzuri kesho kama njia ya kuthamini upendo na sapoti yao,”




