Kuogelea

TSA yafurahishwa na mashindano ya vijana, waogeleaji wapata nafasi timu ya taifa

DAR ES SALAAM:UONGOZI wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) umeeleza kufurahishwa na mafanikio ya Mashindano ya Klabu za Vijana wenye umri wa miaka sita hadi 12, yaliyowezesha baadhi ya waogeleaji kuchaguliwa kujiunga na timu ya taifa ya vijana.

Mashindano hayo yalimalizika katika bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya IST, Masaki, jijini Dar es Salaam, yakishirikisha waogeleaji 400 kutoka Tanzania, Kenya na Zambia.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TSA, David Mwasyoge, amesema mashindano hayo yamekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kiwango kizuri kilichoonyeshwa na washiriki.
“Tunashukuru mashindano haya yamemalizika kwa mafanikio makubwa.

Baadhi ya waogeleaji wamechaguliwa na Kamati ya Ufundi kujiunga na timu ya taifa ya vijana itakayoshiriki Mashindano ya Kanda ya Tatu yatakayofanyika Uganda mwezi Oktoba mwaka huu,” amesema Mwasyoge.

Ameongeza kuwa uteuzi huo umetokana na viwango bora vilivyoonyeshwa na waogeleaji hao pamoja na maendeleo ya nyakati zao za ushindani.

Mwasyoge amesema ushindani ulikuwa mkubwa, hasa kutoka Klabu ya Bandari ya Kenya, ambayo ilionesha kiwango cha juu, lakini vijana wa Tanzania waliweza kukabiliana vyema na changamoto hiyo.
“Klabu ya Bandari imeonyesha ushindani mkubwa.

Tunafurahi kuona vijana wetu wakikabiliana na changamoto hiyo kwa ujasiri. Pia nawapongeza wazazi ambao wamekuwa bega kwa bega nasi katika maendeleo ya mchezo huu,” amesema.

Aidha, amewataka wadhamini kuendelea kuunga mkono mashindano ya kuogelea kwa kuwa ni jukwaa muhimu la kuibua na kukuza vipaji vya vijana nchini.

Kwa upande wake, Kocha wa Klabu ya Bandari kutoka Kenya, Abdalla Mansour, amesema mashindano hayo yalikuwa na ushindani mkubwa, lakini waogeleaji wake walifanikiwa kujinyakulia baadhi ya medali.

“Haikuwa rahisi kwa sababu ushindani ulikuwa mkubwa. Hata hivyo, vijana wetu wamepambana na kupata baadhi ya medali.

Pia tunashukuru kwa ukarimu mkubwa tulioupata Tanzania,” amesema Mansour.

Ameongeza kuwa timu yake itarejea Kenya kujipanga upya kwa ajili ya mashindano yajayo, akilenga kupata matokeo bora zaidi.

Related Articles

Back to top button