Klabu ya kuogelea HPT yang’ara Dubai

KLABU ya Kuogelea ya HPT kutoka Tanzania imeshika nafasi ya 36 ikijizolea jumla ya pointi 360 baada ya wachezaji wake kujitahidi kufanya vizuri katika mashindano ya wazi ya Dubai yaliyomalizika jana.
Zaidi ya klabu 127 kutoka mataifa mbalimbali zilishiriki mashindano hayo na washiriki zaidi ya 1300 walishindana na kuondoka na medali mbalimbali.
Wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo walikuwa ni Sebastian Carpintero, Kaysan Kachra, Konhelli Mhella na Crissa Dillip.
Medali zilizopatikana katika michuano hiyo zilibebwa na Crissa aliyepata medali ya fedha katika mbio za mita 50 mtindo wa Backstroke na medali ya shaba mbio za mita 200 Backstroke.
Kwa mujibu wa Kocha Alexander Mwaipasi, kikosi kilionesha kiwango kizuri na wengi wameboresha muda wao wa kuogelea.