Vijay astaafu uigizaji rasmi

MUMBAI: Mwigizaji maarufu wa India, Vijay, ameaga rasmi tasnia ya filamu baada ya zaidi ya miongo mitatu ya mafanikio, huku filamu yake ya mwisho ‘Jana Nayagan’ ikizinduliwa leo na kuamsha hisia kali miongoni mwa mashabiki duniani.
Hashtag ya #OneLastTime imekuwa miongoni mwa zinazotrendi kwenye mitandao ya kijamii, ambapo mashabiki wamekuwa wakimpongeza kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya filamu za Kitamil na kumtakia kila la heri katika safari yake mpya ya kisiasa.
Vijay, ambaye amejijengea umaarufu kupitia filamu nyingi zilizovunja rekodi za mauzo, amethibitisha kuwa anaweka kando taaluma ya uigizaji ili kujikita kikamilifu katika shughuli za kisiasa kupitia chama chake kipya.
Kutolewa kwa ‘Jana Nayagan’ kumekuwa tukio kubwa nchini India, huku mamia ya mashabiki wakikusanyika katika kumbi mbalimbali za sinema tangu alfajiri kushuhudia kazi hiyo inayotajwa kuwa hitimisho la safari yake ya kipekee kwenye ulimwengu wa filamu.
Wadau wa burudani wanasema uamuzi wa Vijay unaashiria mwisho wa enzi kwa mmoja wa waigizaji waliofanikiwa zaidi katika historia ya sinema za India, baada ya kutamba kwa miaka mingi kwa filamu zilizotikisa soko la ndani na kimataifa.
Katika kipindi chote cha kazi yake, Vijay ameshinda tuzo mbalimbali na kujenga msingi mkubwa wa mashabiki, jambo lililomfanya kuwa miongoni mwa nyota wenye ushawishi mkubwa nchini India.
Mashabiki wengi wameeleza kuwa, licha ya kusikitishwa na uamuzi wake wa kuacha uigizaji, wanaunga mkono hatua yake ya kuanza ukurasa mpya wa maisha katika siasa, wakiamini ataendelea kutoa mchango kwa jamii kupitia jukwaa hilo.
Filamu ya ‘Jana Nayagan’ inatarajiwa kuvutia mamilioni ya watazamaji ndani na nje ya India, huku ikiwa kumbukumbu ya mwisho ya safari ya mmoja wa mastaa wakubwa kabisa wa filamu za Kitamil.




