Michezo Mingine

Klopp akabidhiwa Ujerumani

BERLIN: Chama cha Soka cha Ujerumani (DFB) kimemteua rasmi Jürgen Klopp kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa.

Rais wa DFB, Bernd Neuendorf, ameeleza hayo leo Ijumaa akifafanua kuwa uongozi wa chama hicho uliridhia kwa kauli moja uteuzi wa Klopp, huku akimtaja kama chaguo mwafaka kwa nafasi hiyo.

Klopp anarithi mikoba ya Julian Nagelsmann aliyejiuzulu kufuatia kupoteza kwa mikwaju ya penalti 4-3 katika hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Paraguay.

“Ni heshima kubwa kuwepo hapa leo. Hakika nimefurahishwa sana,” alianza kueleza Klopp punde baada ya kutambulishwa.

“Timu ya taifa inaweza kutuunganisha sisi Wajerumani kwa namna ambayo karibu hakuna kitu kingine kinachoweza kufanya hivyo. Hilo ndilo hasa linalofanya jukumu hili kuwa la kipekee kwangu,” alisema Klopp.

Alisema anatarajia changamoto ya kipekee katika soka la Ujerumani, waikabili pamoja na mashabiki, kwa unyenyekevu na subira, wakati akijenga timu inayopigania ushindi na kufurahia kucheza soka.

Mkataba wa kocha huyo wa zamani wa Liverpool, utaanza Agosti 15, mwaka huu hadi majira ya joto ya mwaka 2030, wakati wa michuano ijayo ya Kombe la Dunia.

Mechi yake ya kwanza kama kocha mkuu wa Ujerumani itakuwa Septemba 24 dhidi ya Uholanzi, ukiwa ni mchezo wa ufunguzi wa Ujerumani katika michuano ya Nations League.

Hii ni kazi ya kwanza ya ukocha kwa Klopp tangu alipoondoka Liverpool mwaka 2024 kutokana na uchovu baada ya kudumu nayo kwa misimu tisa.

Pia, DFB imemtangaza nyota wa zamani wa Arsenal, Per Mertesacker atakuwa mkurugenzi wake mkuu, baada ya mtangulizi wake, Andreas Rettig, kuondoka katika wadhifa huo mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa sasa Mertesacker aliyekipiga Werder Bremen na Hannover 96, anakinoa kikosi cha Akademi ya Arsenal.

 

Related Articles

Back to top button