Promota asikitishwa Diamond Platnumz kutotumbuiza Kenya

NAIROBI: MUANDAAJI wa Tamasha la Furaha City, Willis Raburu amezungumzia kutokuwepo kwa Diamond Platnumz kwenye tukio hilo katika taarifa yake ya kina aliyoichapisha kwenye akaunti yake rasmi ya X, jana Desemba 8, 2024.
Raburu amesema kuwa licha ya jitihada kubwa za kumhudumia nyota huyo wa Tanzania na timu yake, madai na mwenendo wao umekatisha tamaa.
“Tunasikitika sana kutangaza kwamba Diamond Platnumz hakutumbuiza kwenye tamasha la Furaha City kama ilivyopangwa. Kama waandaaji, tulifanya kila jitihada kumgharamia yeye na timu yake na kuhakikisha kwamba mipango na dharura zote zimewekwa kwa ajili yake,” Raburu amesema.
Amesisitiza kuwa ingawa waandaaji wanaheshimu hadhi ya Diamond Platinumz kama msanii wa kiwango cha juu, weledi na kuheshimiana ni muhimu katika ushirikiano huo.
Raburu aliwahakikishia mashabiki kwamba timu imejitolea kusuluhisha suala hilo kwa amani na kujifunza kutokana na uzoefu ili kuhakikisha mafanikio makubwa kwa matoleo yajayo ya tamasha hilo.
Raburu pia alikubali suala dogo la usalama lililohusisha msanii mwingine wakati wa hafla hiyo, ambalo lilitatuliwa haraka ili kuhakikisha onyesho linaendelea vizuri na kwa weledi.
Katika taarifa yake, Raburu aliwasifu wasanii waliotumbuiza, akiangazia nguvu na weledi wa kipekee walioonyeshwa na wanamuziki wa Kenya, pamoja na maonyesho ya wasanii wa Wasafi Zuchu na Rayvanny, ambao walitoa seti za kukumbukwa.
“Tunajivunia sana maonyesho ya ajabu yaliyotolewa na wasanii wengine wote. Wasanii wa Kenya walijipambanua, wakionyesha talanta na nishati isiyo na kifani ili kuwapa watazamaji shoo isiyoweza kusahaulika,” ameeleza.
Jibu la Raburu linakuja baada ya waliohudhuria kueleza kusikitishwa na kitendo cha Diamond kutohudhuria hafla hiyo.