Mitindo

Miss Universe Tanzania 2026 yazinduliwa

DAR ES SALAAM: Mashindano ya urembo Miss Universe Tanzania 2026 yamezinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam, huku waandaaji wakiahidi kuandaa msimu mkubwa zaidi tangu walipopata haki ya kuendesha mashindano hayo nchini.

Msimu wa mwaka huu umebeba kaulimbiu ya “Nishati Safi Jikoni”, ikiwa na lengo la kuwawezesha wanawake kupitia uongozi, ujasiriamali, utamaduni na utalii.

Washiriki watapata mafunzo mbalimbali, kushiriki ziara katika mikoa tofauti na kupewa fursa ya kukuza uwezo wao kabla ya kuwania taji hilo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkurugenzi wa Miss Universe Tanzania, Millen Magese, alisema ushirikiano na Azam TV utawapa Watanzania nafasi ya kufuatilia safari nzima ya mashindano kupitia kipindi cha Reality TV.

Kipindi hicho kitaonesha hatua zote kuanzia usaili wa washiriki, mafunzo kambini, maandalizi ya fainali, safari ya kutafuta taji hadi maisha ya mshindi baada ya ushindi.

Kwa upande wake, Miss Universe Tanzania 2025, Naisae Yona, amesema mashindano hayo yameleta mabadiliko makubwa katika maisha yake kwa kumjengea ujasiri, kujiamini na kujitambua zaidi.

Amewahimiza wasichana wenye ndoto za kushiriki kutoruhusu hofu kuwazuia kufikia malengo yao.

Usaili wa washiriki unatarajiwa kufanyika kuanzia Julai 25 hadi 27, huku fainali ya Miss Universe Tanzania 2026 ikipangwa kufanyika Septemba 5.

Mshindi wa taji hilo atapata heshima ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss Universe 2026 yatakayofanyika nchini Puerto Rico.

Related Articles

Back to top button