Mastaa

Meja Kunta aishukuru serikali, wasanii na mashabiki baada ya msiba wa baba yake

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Singeli, Meja Kunta, ametoa shukrani za dhati kwa Watanzania wote walioshiriki na kumuunga mkono katika kipindi cha msiba wa baba yake, aliyepumzishwa jana katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo kupitia ukurasa wa istagram, Meja Kunta ameandika ameguswa na upendo mkubwa, faraja na msaada alioupata kutoka kwa ndugu, marafiki, mashabiki pamoja na wadau mbalimbali wa tasnia ya muziki na burudani tangu baba yake alipopata matatizo ya kiafya hadi alipofariki na kuzikwa.

“Ndugu, marafiki na wote mlionisimamia, ninawashukuru kwa dhati kwa upendo, msaada na faraja mlionipa katika kipindi hiki kigumu cha kumpumzisha baba yangu.

“Uwepo wenu, michango yenu, sala zenu na maneno yenu ya kutia moyo vimenipa nguvu kubwa. Naomba Mwenyezi Mungu awalipie mema kwa kila jambo mlilonitendea, awazidishie afya, riziki na kuwalinda pamoja na familia zenu,” ameandika Meja Kunta.

Mbali na hilo, msanii huyo ameishukuru serikali, hususan Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa mchango wake katika kuratibu na kufanikisha matibabu ya baba yake kabla ya kifo chake.

Pia ametoa shukrani kwa wadau wa tasnia ya michezo na burudani waliokuwa bega kwa bega naye kuanzia kipindi cha matibabu hadi siku ya mazishi, akisema ushirikiano wao umeonyesha mshikamano mkubwa ndani ya sekta hiyo wakati wa kipindi kigumu cha maombolezo.

Related Articles

Back to top button