Mastaa

Naya aendeleza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi

MWIGIZAJI maarufu wa filamu kutoka Nigeria, Beverly Naya, amesema makala yake ya mwaka 2019 yenye jina la SKIN ililenga kuhamasisha jamii kupinga ubaguzi wa rangi ya ngozi (colorism) na tabia ya wanawake kujichubua ngozi ili kufikia viwango vinavyodhaniwa kuwa vya urembo.

Naya amesema aliamua kutengeneza makala hiyo baada ya kushuhudia athari za ubaguzi wa rangi ya ngozi nchini Nigeria, akieleza kuwa wanawake wengi hujikuta wakijichubua kwa kuamini kuwa ngozi nyeupe ndiyo ishara ya uzuri na kukubalika katika jamii.

Kwa mujibu wa mwigizaji huyo, tatizo hilo ni kubwa nchini Nigeria, ambapo alidai kuwa takribani asilimia 77 ya wanawake hujihusisha na vitendo vya kujichubua ngozi kutokana na shinikizo la kijamii na unyanyapaa unaowakumba wenye ngozi nyeusi.

Aidha, amesisitiza kuwa matumizi ya majina ya kubeza kama “Blackie” kwa watu wenye ngozi nyeusi ni aina ya ubaguzi unaoumiza hisia na unaopaswa kukomeshwa.

“Nilitengeneza SKIN kupinga viwango vya urembo vinavyowasukuma wanawake wengi kuamini kuwa ngozi nyeupe ndiyo inayovutia zaidi. Mtazamo huo si mzuri na unapaswa kubadilika,” amesema Naya.

Kauli yake imeibua mjadala mpana kuhusu mtazamo wa jamii juu ya rangi ya ngozi na umuhimu wa kukubali uzuri wa asili bila kujali rangi ya mtu.

Je, bado unaamini kuwa ngozi nyeupe ndiyo kipimo cha uzuri, au ni wakati wa kuthamini uzuri wa asili katika rangi zote za ngozi?

Related Articles

Back to top button