
BUDAPEST: Bingwa mara saba wa dunia wa mbio za Formula One, Lewis Hamilton, amesema anajivunia mafanikio aliyoyapata pamoja na timu yake ya Ferrari kufanikiwa kuinuka kutoka katika kipindi kigumu alichokipitia mwaka mmoja uliopita.
Hamilton, mwenye umri wa miaka 41, alikumbuka mashindano ya Hungarian Grand Prix ya mwaka jana ambapo alijikosoa vikali baada ya kufanya vibaya katika hatua za mchujo na kumaliza mbio katika nafasi ya 12, huku akijieleza kuwa hana msaada hata kupendekeza Ferrari imsajili dereva mwingine.
Akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi, Hamilton alisema safari yake ya kurejea kwenye kiwango bora imekuwa ya kujivunia.
“Ninajivunia kila mmoja ndani ya timu na pia ninajivunia mimi mwenyewe kwa jinsi nilivyoweza kujitoa katika hali ile ngumu niliyokuwa nayo. Siku moja nitakapotoa makala yangu ya maisha, nitasimulia kila kilichotokea mwishoni mwa wiki ile. Leo niko mbali sana na nilipokuwa mwaka jana,” alisema Hamilton.
Msimu huu, Hamilton amekuwa katika kiwango kizuri na anashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa madereva akiwa nyuma kwa pointi 45 ya kijana wa Mercedes mwenye umri wa miaka 19, Kimi Antonelli.
Dereva huyo wa Ferrari tayari amepanda jukwaani mara tano msimu huu, ikiwemo ushindi wake wa kwanza akiwa na Ferrari alioupata nchini Hispania, mafanikio ambayo yameongeza matumaini ya timu hiyo kurejea kwenye ushindani wa ubingwa.
Hamilton alisema maendeleo ya Ferrari yametokana na kazi kubwa ya pamoja huku akiisifu timu kwa kuboresha gari na kuongeza ushindani katika kila mbio.
“Ninashukuru kwa jinsi tulivyokua kama timu. Vipande vya mafanikio vinaendelea kuunganishwa na sasa tuna gari zuri pamoja na kifurushi bora kinachotuwezesha kupambana kwa ushindi,” alisema.
Macho sasa yanaelekezwa kwenye mbio za Hungarian Grand Prix zitakazofanyika Jumapili, ambapo Hamilton ana rekodi bora katika uwanja huo baada ya kushinda mara nane, kuanza mbio kutoka nafasi ya kwanza mara tisa na kuongoza mizunguko 487, rekodi ambayo haijavunjwa na dereva mwingine katika uwanja mmoja.
Iwapo atafanikiwa kushinda mbio hizo, Hamilton ataongeza rekodi yake ya ushindi hadi mara 107 katika historia ya Formula One na kuimarisha nafasi yake katika mbio za kuwania ubingwa wa dunia msimu huu.



