Tambwe: Yanga na Singida wote ni mafundi

SINGIDA : MENEJA wa timu ya Singida Black Stars na mchezaji wa zamani wa Simba na Yanga, Amis Tambwe, amesema kikosi chao kiko tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga utakaopigwa kesho, akisisitiza kuwa ni pambano la “mafundi” litakalojaa burudani ya soka safi.
Tambwe amesema mkoani hapa kuwa wanautazama mchezo huo kama fursa ya kuonesha ubora wao, akiamini utakuwa wa ushindani mkubwa kwa kuwa timu zote mbili zinacheza mpira wa kuvutia.
“Tunajua tutafanya vizuri katika mchezo huo. Utakuwa mzuri kwa sababu wanakutana mafundi wote, kila upande unacheza mpira mzuri,” amesema.
Tambwe ametoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Airtel mkoani hapa ili kuipa timu hamasa zaidi.
“Tunaomba mashabiki waje kwa wingi watupatie sapoti, wachezaji wetu wajitume zaidi wanapoona nyuma yao kuna nguvu ya mashabiki,” ameongeza.
Kuhusu hali ya kikosi, Tambwe amesema ipo vizuri na wachezaji wako kwenye morali ya juu kuelekea katika mchezo huo.




