Ligi Kuu

Yanga yatua Lindi kuvaana na Namungo

LINDI:MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga, wametua Ruangwa mkoani Lindi tayari kwa mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Namungo utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Majaliwa, huku macho yakielekezwa kuona namna kikosi kipya cha Kocha Manqoba Mngqithi kitakavyoanza safari ya kutetea ubingwa.

Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na morali kubwa baada ya kuifunga Simba bao 1-0 katika Ngao ya Jamii na kutwaa taji hilo kwa mara ya 10, hivyo ikilenga kuendeleza kasi hiyo katika mashindano ya ligi.

Hata hivyo, safari yao ya Lindi inawakutanisha na Namungo yenye morali yake baada ya kutoka kuichapa Polisi Tanzania mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki uliokuwa sehemu ya maandalizi yao kuelekea msimu mpya.

Mchezo huo unakuwa pia mtihani mwingine kwa benchi jipya la ufundi la Yanga, ambalo linatakiwa kuanza kuonesha sura yake katika ligi baada ya timu hiyo kufanya mabadiliko kadhaa katika kikosi na kuongeza wachezaji wapya.

Pamoja na ujio wa wachezaji wapya, Yanga bado ina kundi la wachezaji wenye uzoefu wa kutosha katika ligi na mashindano ya kimataifa, jambo linaloongeza matarajio kwa mashabiki kuona timu hiyo ikianza ligi kwa matokeo mazuri.

Kwa upande wa Namungo, wenyeji nao wamefanya maboresho katika kikosi chao kwa kusajili baadhi ya wachezaji wapya, huku wakiendelea kutegemea pia uzoefu wa wachezaji waliokuwapo ili kuifanya timu iwe na ushindani zaidi.

Rekodi ya msimu uliopita inaipa Yanga matumaini zaidi, kwani katika mechi mbili walizokutana na Namungo, iliondoka na pointi zote sita baada ya kushinda michezo yote miwili.

Katika mchezo wa mwisho uliowakutanisha kwenye Uwanja wa Majaliwa, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0, hivyo Namungo kesho itakuwa na jukumu la kuvunja rekodi hiyo mbele ya mashabiki wake.

Kwa Yanga, ushindi utaifanya ianze msimu kwa hatua nzuri na kuendeleza morali iliyojengwa baada ya kutwaa Ngao ya Jamii, wakati Namungo itakuwa na nafasi ya kuanza ligi kwa kuwatibulia mabingwa mipango yao.

Related Articles

Back to top button