Masumbwi

Bondia Prichard Colón afariki miaka 10 baada ya jeraha la ubongo

PUERTO RICO:BONDIA wa Puerto Rico, Prichard Colón, amefariki dunia akiwa na miaka 33, zaidi ya miaka 10 baada ya kupata jeraha kubwa la ubongo lililobadilisha maisha yake kufuatia pambano la ndondi mwaka 2015.

Colón alipata jeraha hilo wakati akipambana na Terrel Williams mwaka 2015, katika pambano lililokuwa la kwanza kwake kupoteza katika taaluma yake ya ndondi.

Wakati wa pambano hilo, Colón alipigwa mara kadhaa nyuma ya kichwa, eneo ambalo ni kinyume na sheria za ndondi. Baada ya pambano, hali yake ilizidi kuwa mbaya na baadaye akapatwa na uvujaji wa damu kwenye ubongo.

Bondia huyo alikaa kwenye koma kwa siku 221, sawa na zaidi ya miezi saba, kabla ya kuamka. Hata hivyo, hakuwahi kupona kikamilifu kutokana na uharibifu mkubwa wa ubongo alioupata.

Tangu wakati huo, Colón alihitaji uangalizi wa muda wote na familia yake iliendelea kuwa karibu naye na kumhudumia kwa miaka yote iliyofuata.

Colón alikuwa bado kijana mwenye umri wa miaka 22 wakati tukio hilo lilipotokea. Alikuwa ameanza kujijenga kwenye ndondi za kulipwa, lakini pambano hilo likabadilisha kabisa maisha yake.

Kabla ya pambano lake hilo la mwisho,Colón alikuwa amepigana mara 16,akishinda mapambano yote,huku mapambano 13 yakiwa ni ya Knock Out (KO).

Related Articles

Back to top button