Simba Queens wana balaa hao!
DAR ES SALAAM: TIMU ya Simba Queens imetinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kawempa Muslim ya Uganda.
Katika mchezo huo uliopigwa katika leo Jumatano Agosti 21 Uwanja wa Abebe Bikila, Ethiopia, timu hizo zilienda mapumziko zikiwa hazijafungana kutokana na ubora waliokuwa nao Kawempe, uliochangiwa na hali ya hewa ya baridi kali kwa wachezaji wa Simba.
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Vivian Corazone aliwapatia bao la kwanza dakika ya 64 kwa kichwa baada ya kumalizia mpira wa kona uliopigwa na Precious Christopher.
Dakika tano baadae Jentrix Shikangwa aliwapatia bao la pili kwa kichwa akimalizia mpira wa kona iliyopigwa na Precious huku Elizabeth Wambui alikamilisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la tatu dakika ya 75 kwa shuti lilomshinda kipa wa Kawempa, Adeke Juliet.
Ushindi huo umewapa Simba tiketi ya moja kwa moja ya kucheza nusu fainali ambapo mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya PVO Bunyenzi ya Burundi, utakaopigwa Agosti 23 utakuwa wa kukamilisha ratiba.
Kocha Mkuu wa Simba Queens, Juma Mgunda amesema wamejianda kwa ajili ya kufanya vizuri katika michuano hiyo ya CECAFA kutafuta tiketi ya kwenda kuwakilisha ukanda huo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.