Afrika Mashariki

Mariga aeleza alivyoshindwa kucheza EPL

NAIROBI: KIUNGO wa zamani wa Kenya, McDonald Mariga, ameelezea tena jinsi ndoto yake ya kuwa Mkenya wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England ilivyovunjika miaka 16 iliyopita.

Mariga alizungumzia kwa mara nyingine kuhusu uhamisho wake ulioshindikana kwenda klabu ya Manchester City mwaka 2010.

Mnamo Januari mwaka huo, alikuwa karibu kuandika historia baada ya City, iliyokuwa chini ya kocha Roberto Mancini, kukubaliana na klabu yake ya Parma kuhusu dili la uhamisho. Mkataba ulikuwa tayari umeandaliwa na makubaliano kufikiwa, lakini mambo yaliharibika dakika za mwisho.

Sababu ya kuvunjika kwa dili hilo ilikuwa ni jopo la Uingereza kukataa uhamisho wake kutokana na nafasi ya chini ya Kenya katika viwango vya FIFA, ambapo sheria zilihitaji mchezaji atoke katika nchi iliyo ndani ya nafasi 70 bora duniani hali ambayo Kenya haikutimiza wakati huo.

Kutokana na hilo, Mariga alishindwa kupata kibali cha kazi nchini Uingereza. Hata juhudi za serikali ya Kenya, kupitia aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo Raila Odinga, hazikuweza kubadilisha uamuzi huo.

Akizungumza katika mahojiano, Mariga alisema:
“Nilisaini na Man City lakini kulikuwa na jopo lililokuwa linaamua nani aruhusiwe kucheza. Kulikuwa na sheria kwamba timu ya taifa lazima iwe ndani ya 70 bora duniani, lakini sisi tulikuwa kama nafasi ya 130, hivyo sikufuzu.”

Aliongeza kuwa kati ya wajumbe saba wa jopo hilo, watatu walikubali acheze lakini wanne walipinga, jambo lililofanya dili hilo kufeli.

“Nilikuwa tayari nimeshasaini mkataba. Nilirudi Italia, wao wakamsajili Patrick Vieira, na mimi nikajiunga na Inter Milan,” alisema.

Licha ya pigo hilo, Mariga anasema kushindwa huko kuligeuka kuwa baraka, kwani alijiunga na Inter Milan chini ya kocha Jose Mourinho.

Akiwa hapo, alipata mafanikio makubwa ndani ya miezi sita tu, huku Inter ikishinda mataji matatu makubwa Ligi Kuu ya Italia, Kombe la Italia na UEFA Champions League mwaka 2010.

Kwa ujumla, Mariga alicheza mechi 36 akiwa Inter na kushinda mataji sita, kabla ya kurejea Parma baada ya mkopo katika klabu ya Real Sociedad.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button