Nyumbani

Shime: Hatutarudia Makosa Ugenini

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake Twiga Stars, Bakari Shime, amesema kikosi chake kitafanya vizuri zaidi kwenye mchezo wa marudiano wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 dhidi ya Equatorial Guinea.

Twiga Stars ilianza vyema kwa kushinda mabao 3-1 dhidi ya Equatorial Guinea katika mchezo wa kwanza uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam.

Shime amesema mchezo huo ulikuwa mgumu na walifanya makosa kwa kuruhusu bao, kabla ya kurekebisha makosa hayo na kuibuka na ushindi.

“Tulishindwa kukaa vizuri katika eneo letu, hasa kwa washambuliaji. Hii ilitokana na baadhi ya wachezaji kufika kambini siku moja kabla ya mechi na kuingia moja kwa moja uwanjani.

“Nina imani siku hizi tunazoendelea kujiandaa zitawasaidia wachezaji kuingia kwenye mbinu zetu na hawatakuwa na uchovu wa safari kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza. Mechi inayofuata itakuwa bora zaidi,” amesema.

Akizungumzia mchezo wa jana, Shime amesema baada ya kuruhusu bao walichambua makosa yao na kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Asnat na Aisha, kisha kuwaingiza Enekia na Stumai Abdallah.

“Mabadiliko hayo yalitusaidia kupata mabao mawili haraka na kuongeza la tatu. Tulikuwa hatujawafahamu vizuri wapinzani wetu, lakini sasa tuna picha yao kamili. Nadhani mechi ijayo tutafanya vizuri zaidi. Tunahitaji kushinda ugenini ili kuhakikisha tunafuzu WAFCON 2026,” amesema.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button