Serikali imetenga bilioni 76 kwa AFCON 2027

DODOMA: SERIKALI imetenga dola milioni 30 (zaidi ya Shilingi bilioni 76) kwa ajili ya ada ya uandaaji wa mashindano ya AFCON 2027, hatua inayoonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha Tanzania na washirika wake wanafanikisha maandalizi ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Akizungumza bungeni leo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuimarisha maandalizi ya miundombinu na uendeshaji wa mashindano hayo.
Amesema Tanzania imejipanga kikamilifu kushirikiana na nchi washirika katika kuhakikisha AFCON 2027 inafanyika kwa viwango vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuboresha viwanja, barabara, hoteli na huduma nyingine muhimu.
Makonda alibainisha kuwa mafanikio ya mashindano ya CHAN 2024 yameipa Tanzania uzoefu mkubwa na kuonyesha uwezo wa nchi kuandaa mashindano ya kimataifa kwa mafanikio.
Amesema pia timu ya Taifa, Taifa Stars, ilionesha kiwango cha juu kwa kufika robo fainali, jambo linaloashiria maendeleo ya soka la ndani.
Katika maandalizi ya AFCON 2027, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ikiwemo ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa pamoja na ujenzi wa viwanja vipya vya mazoezi nchini.
Makonda amesema uwekezaji huo mkubwa wa fedha na miundombinu ni ishara ya dhamira ya Serikali ya kuhakikisha Tanzania inakuwa mwenyeji bora wa mashindano hayo, huku ikinufaika kiuchumi kupitia utalii na biashara.




