Isarito awakaribisha wageni kutembelea vivutio vya utalii Tanzania

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu nchini, Isarito Mwakalindile, amewakaribisha wageni kutoka mataifa mbalimbali kutembelea Tanzania, akieleza kuwa nchi ina amani, vivutio vya kipekee vya utalii na mazingira rafiki yanayowawezesha wageni kufurahia uzuri wa maliasili, utamaduni na ukarimu wa Watanzania.
Akizungumza na SpotiLeo, Isarito amesema Tanzania ni miongoni mwa mataifa yenye amani na utulivu mkubwa barani Afrika, hali inayowapa wageni nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii kwa uhuru na usalama.
“Tanzania ni nchi ya amani. Mgeni anaweza kutembelea sehemu mbalimbali kwa uhuru na kufurahia vivutio vya utalii, tamaduni zetu pamoja na burudani zinazopatikana katika maeneo tofauti ya nchi,” amesema.
Ameeleza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya asili vinavyovutia watalii kutoka duniani kote, ikiwemo mbuga za wanyama, milima, fukwe za bahari, maeneo ya kihistoria pamoja na tamaduni mbalimbali za Kitanzania.
Aidha, amewahimiza wageni watakaoshiriki matukio mbalimbali ya kimataifa nchini, ikiwemo AFROCON, kutotumia muda wao kufuatilia michezo pekee, bali watenge muda wa kutembelea maeneo ya utalii na kujifunza historia, utamaduni na urithi wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Isarito, hatua hiyo itasaidia kukuza sekta ya utalii, kuongeza mapato ya nchi na kuendelea kuitangaza Tanzania kama moja ya maeneo bora ya kutembelea barani Afrika.
Msanii huyo pia amesisitiza umuhimu wa wasanii kushiriki katika kuitangaza Tanzania kimataifa, akibainisha kuwa sanaa ni jukwaa kubwa linaloweza kufikisha ujumbe kwa watu wengi duniani na kusaidia kuvutia watalii zaidi nchini.
“Tunapaswa kutumia majukwaa yetu kuitangaza Tanzania. Sanaa ina nguvu kubwa ya kuifikisha nchi yetu kwa watu wengi zaidi na kusaidia kukuza utalii pamoja na uchumi wa taifa,” amesema.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya sekta ya sanaa na utalii unaweza kuwa chachu ya maendeleo makubwa, huku ukiendelea kuitangaza Tanzania kama taifa lenye amani, vivutio vya kipekee na watu wenye ukarimu mkubwa.




