Saadun aondoka Stars kisa Yanga
DAR ES SALAAM: Mshambuliaji wa Azam FC, Nassor Saadun ameondoka kambi ya Taifa Stars inayojianda na mchezo wa mkondo wa pili wa kufuzu michuano ya CHAN dhidi ya Sudan, mchezo utakaopigwa Novemba 03, mwaka huu.
Ofisa habari wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo ameweka wazi kuwa uongozi wa Azam FC umeomba mchezaji huyo kurejea kikosini kwa ajili ya kusaidia timu yake katika mchezo wa dhidi ya Yanga.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi Novemba 02, Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi nje kidogo ya jiji ambapo Yanga ni wenyeji wa mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Ni kweli tumepokea maombi ya Azam FC ikimuhitaji Saadun kwenda kujiunga na timu yake kucheza dhidi ya Yanga na baada ya mechi hiyo atarejea kambini Stars,” amesema.
Ndimbo amesema wametoa ruhusa hiyo kwa kutambua umuhimu wa mchezo huo na atarejea kuendelea na majukumu ya Taifa katika mchezo wa marudiano dhidi ya Sudan kutafuta nafasi ya kufuzu fainali za CHAN 2025.