Mgunda: Makosa yetu yametugharimu dhidi ya Yanga

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Namungo FC, Juma Mgunda amesema makosa ya kujirudia yaliyofanywa na wachezaji wake ndiyo yaliyoigharimu timu hiyo katika mchezo waliopoteza mabao 3-1 dhidi ya Yanga jana.
Mgunda amesema kucheza dhidi ya timu yenye wachezaji wenye ubora kama Yanga kunahitaji umakini mkubwa kwani kosa dogo linaweza kuadhibiwa haraka.
“Mchezo wowote unapocheza na timu yenye wachezaji wenye ubora, mkifanya makosa ya kurudia mtaadhibiwa. Mabao yote tuliyofungwa yametokana na makosa yetu wenyewe,” amesema Mgunda.
Kocha huyo amesema pamoja na matokeo hayo, anawapongeza wachezaji wake kwa kujituma ndani ya uwanja, lakini amekiri kuwa walikosa umakini katika baadhi ya maeneo muhimu.
“Vijana wamejitahidi kucheza, lakini makosa tuliyofanya ya kujirudia yametuadhibu,” amesema.
Mgunda amesema kipigo hicho kinaumiza, lakini kama kocha mkuu anabeba jukumu la kuhakikisha makosa hayo yanafanyiwa kazi kabla ya michezo ijayo.
“Kufungwa inauma na inagusa. Utaona ni makosa ya mtu mmoja mmoja, lakini mimi kama mwalimu nayabeba na kwenda kuyafanyia kazi,” amesema.
Ameongeza kuwa mapumziko ya wiki mbili yajayo yataitumiwa na benchi la ufundi kuifanyia maboresho timu hiyo kabla ya kurejea kwenye michezo iliyobaki ya ligi.
“Kuna wiki mbili za mapumziko, tutakwenda kujitayarisha kwa mechi tano zijazo kuhakikisha tunafanya vizuri,” amesema.
Mgunda pia aliwatetea wachezaji wake akieleza kuwa hakuna aliyefanya makosa kwa makusudi bali ni sehemu ya mchezo, huku akiahidi kuzungumza nao ili kuongeza umakini zaidi.
“Hakuna mchezaji anayeingia uwanjani kufanya makosa ya kukusudia, imetokea tu. Ni wanangu, nitazungumza nao kuongeza umakini,” amesema.




