Ratiba ya Ligi kuu hadharani Agosti 2, Simba Vs Yanga lini?
DAR ES SALAAM: AGOSTI 2, mwaka huu ndio siku klabu kongwe nchini, Simba na Yanga watafahamu lini watakua katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya Ofisa ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ligi kuu Tanzania Bara (TPLB), Almas Kasongo kutaja siku hiyo wanatarajia kutangaza ratiba ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024/25, ambao utaanza rasmi Agosti 16, mwaka huu.
Simba na Yanga wanakutana katika mchezo wa Ngao ya Hisani utakaochezwa Agosti 8, mwaka huu lakini wengi wanasubiri kuona na kusikia watani hao wanakutana lini katika mchezo wa ligi kuu na nani anakuwa nyumbani na ugenini.
Akizungumza na Spotileo, Kasongo amesema baada ya kumalizika kwa msimu uliopita walikutana kamati ya utenda ya TPLB na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kujielekeza kuandaa kalenda ya msimu 2024/25.
Amesema walikuwa rasimu nyingi kwa ajili ya kupanga ratiba ya msimu wa 2024/25 hadi kufikia hatua ya mwisho ya kuipata ratiba bora na kuona namna gani ya kuondokana na changamoto nyingi za jiratiba za msimu uliopita.
“Kwa hiyo tukajiridhisha kuwa kila kitu kipo vizuri na ratiba ni rafiki, imeakisi changamoto tulizopitia msimu uliopita, sasa tutakuwa tayari kuitangaza na tunatarajia Agosti 2, mwaka huu kuiweka hadharani.
Ratiba yetu imezingatia kalenda za Shirikisho la Soka Ulimwenguni Fifa na CAF kwa kutoingilia michuano ya Kimataifa kwa klabu zetu zinazoshiriki, timu zetu za Taifa katika kalenda ya Fifa ikiwemo mashindano na michezo ya kirafiki,” amesema Kasongo.