Ligi Kuu

Azam FC kujipima mechi mbili za kirafiki

DAR ES SALAAM: KIKOSI cha Azam FC, kinachonolewa na kocha Rachid Taoussi, kipo katika maandalizi kabambe kuelekea kurejea kwa Ligi Kuu Tanzania Bara. Timu hiyo tayari imeanza mazoezi tangu Jumatatu, Machi 17, huku ikipanga kucheza mechi mbili za kirafiki kabla ya kurejea dimbani kwa mchezo wao wa ligi dhidi ya Kengold FC, utakaopigwa Aprili 3, kwenye Uwanja wa Sokoni, Mbeya.

Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabit Zakaria, timu hiyo inatumia mapumziko ya ligi kuimarisha timu yake kupitia michezo ya kirafiki.

“Ni kawaida yetu kucheza mechi za kirafiki pale ligi inapokuwa imesimama. Wiki iliyopita tulicheza mechi moja, na kabla ya kwenda Mbeya tutakuwa na mechi mbili zaidi, mojawapo ikipigwa Jumamosi, Machi 22,” alisema Zakaria.

Kocha Taoussi anatumia michezo hii kama sehemu ya kujifunza na kurekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye michezo iliyopita. Lengo ni kuhakikisha kikosi chake kipo katika hali bora kabla ya kurejea kwenye ushindani wa ligi.

Kwa mashabiki wa Azam FC, macho yote sasa yanaelekezwa kwenye mechi hizi za kirafiki ili kuona namna kikosi kinavyoimarika kuelekea mchezo muhimu dhidi ya Kengold FC

Related Articles

Back to top button