Ligi Ya Wanawake

Rais Samia atoa Mil 30 kwa Serengeti Girls

DAR ES SALAAM:RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Sh milioni 30 kwa timu ya wasichana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Girls’, baada ya kutwaa Ubingwa wa UNAF U-17 ( Timu za Kaskazini mwa Afrika) michuano iliyofanyika nchini Tunisia na Tanzania kualikwa.

Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro amewakabidhi fedha hizo leo jijini Dar es Salaam.

Ndumbaro amewataka wachezaji hao kujituma na kupambana ili kupata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kwa ajili ya kujenga timu ya taifa imara ya wanawake.

“Rais Samia amefurahishwa sana na ushindi huo na kutoa zawadi ya Mama kwa kutoa kiasi cha Sh milioni 30, kwa kuwakabidhi 10 na kesho (Alhamisi, Agosti 12) tutawamalizia 20 kwa sababu mfumo umetukwamisha,” amesema.

Ndumbaro amesema wamepewa maelekezo kwa Rais Samia kuwa wahakikishe timu zote za Taifa zinafanikiwa kufuzu fainali za AFCON pamoja na Kombe la Dunia.

“Tunahakikisha hatutamuangusha Rais Samia na kushirikiana vizuri na TFF ili kufanikisha kile kinachotarajiwa, tungependa kuona wachezaji hao wakipata nafasi ya kucheza soka la kulipwa nje kwa manufaa ya taifa ya baadae,” amesema Ndumbaro.

Wakati huo huo, Waziri Ndumbaro amewapa baraza timu ya wasichana U – 15 ambao wanaenda nchini Bosnia katika mashindano ya soka ya maendeleo ya vijana.

Amesema Tanzania kuna uwepo hai wa timu za Taifa kuanzia U-15 na kuendelea na mchezaji kuitwa kwa timu ya taifa ni heshima kubwa sana na kuilinda heshima hiyo ni kupitia kufanya vizuri uwanjani.

 

Related Articles

Back to top button