‘Yanga Princess kazeni wanangu’

DAR ES SALAAM: BAADA ya kushinda Kariakoo Derby ya Wanawake, Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, amewataka wachezaji wa Yanga Princess kutobweteka na ushindi huo dhidi ya Simba Queens na badala yake waendelee kupambana kwa ajili ya nembo ya klabu hiyo.
Yanga Princess walikuwa ugenini katika mchezo huo uliopigwa Jumanne, Machi 18, kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, jijini Dar es Salaam, na wakaibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao wakuu, Simba Queens.
Arafat amesema anafahamu kuwa ushindi huo ni wa kihistoria na wachezaji wana furaha, lakini bado safari ni ndefu, hivyo wanapaswa kuona huu kama mwanzo mzuri wa kufanikisha malengo waliyojiwekea.
“Tukumbuke hatuchezi kwa ajili yetu binafsi bali kwa mamilioni ya Wananchi wanaoihodhi hii nembo. Tunapambana kwa ajili ya ndoto za mabinti wengine na kwa heshima ya wote waliovuja jasho tangu uhuru kwa ajili ya nembo hii ya Wananchi,” amesema Arafat.
Aidha, amesisitiza kuwa kikosi cha Yanga Princess kina wachezaji chipukizi wenye vipaji na morali kubwa, hivyo wanapaswa kusonga mbele hatua kwa hatua huku wakiheshimu mchakato na kuwa na nidhamu katika kila hatua.
“Tucheze kwa ajili ya nembo kifuani, kisha watatukumbuka kwa majina yetu nyuma ya jezi bado hatujafika, lakini mwelekeo ni mzuri, pongezi kwa benchi la ufundi, wachezaji, viongozi na mashabiki wote mliojitokeza uwanjani,” amesema.