Mastaa

Profesa Jay: Familia iliuza mali zangu nilipokuwa nikipigania uhai wangu

DAR ES SALAAM: RAPA na mwanasiasa nchini Tanzania Joseph Haule ‘Professor Jay’ amefichua kuwa familia yake iliuza mali zake alipokuwa amelazwa akipigania maisha yake na sasa ameamua kuanza upya.

“Ninaanza upya. Tangu nilipougua, ndugu zangu waliuza mali zangu nyingi ili kuokoa maisha yangu. Sijutii kwa sababu jambo muhimu zaidi ni kwamba niko hai leo, hata wakati nafasi za kuishi zilikuwa ndogo. Naweza kujenga tena utajiri wangu,” amesema.

Mbunge huyo wa zamani wa Mikumi ameeleza kuwa mauzo hayo yalifanyika bila yeye kujua, kwani familia yake ilifanya maamuzi kwa niaba yake wakati hajitambui.

“Sikujua walikuwa wakiuza mali zangu. Maamuzi haya yalifanywa na familia yangu kwa vile nilitumia muda wangu mwingi katika hali ya kupigania uhai wangu,” ameongeza.

Profesa Jay aliugua akiwa nyumbani kwake Januari 24, 2022. Mkewe alimkimbiza Hospitali ya Jeshi ya Lugalo kabla ya hali yake kuwa mbaya na hivyo kupelekea kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Alitumia siku 462 hospitalini alipopambania kushindwa kwa figo, shinikizo la damu na ‘cholesterol’ ya juu.

Wakati wa matibabu yake, alikuwa amepoteza fahamu kwa muda mwingi, akitegemea mirija ya kupumua, kula, na kutoka.

Akitafakari uzoefu wake wa kukaribia kufa, Profesa Jay alifichua kwamba alikaa siku 127 ICU na aliambiwa alikuwa na nafasi ya asilimia 40 tu ya kuishi.

“Nilikuwa nimepoteza matumaini kabisa ya kuishi. Nilifikiri ilikuwa ni suala la muda kabla ya kufa,” alisimulia katika mahojiano yaliyotangulia.

Huku akiendelea kupata nafuu, rapa huyo nguli ametangaza nia yake ya kuwania kiti cha Mbunge wa Mikumi katika uchaguzi mkuu wa 2025 nchini Tanzania. Kufikia wakati huo, atakuwa ametimiza miaka 50.

Related Articles

Back to top button