Makonda: Ole wao wanaokiuka katiba

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema baadhi ya viongozi wa mashirikisho ya michezo wamekuwa wakibadilisha katiba za taasisi zao ili kulinda nafasi zao madarakani.
Makonda alitoa kauli hiyo katika mkutano wa Baraza la Michezo la Taifa uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam Leo.
Amesema taarifa alizozipata zinaonesha kuwa wapo viongozi waliokaa madarakani kwa muda mrefu kwa kubadilisha katiba mara kwa mara ili iendane na maslahi yao binafsi.
“Naambiwa kuna watu wamekaa kwenye nafasi miaka zaidi ya 15 kwa kubadilisha katiba kila mara ili iwafae wao kubaki madarakani,” amesema.
Makonda alisisitiza umuhimu wa katiba za mashirikisho kuwa wazi na zenye kulinda maslahi ya wanachama na maendeleo ya michezo badala ya maslahi ya viongozi wachache.
Katika hatua nyingine alihoji, uongozi mpya wa Shirikisho la Kikapu Tanzania (TBF) kwanini hawakabidhiwa ofisi na kuwataka Baraza la Michezo la Taifa BMT ndani ya masaa 24 ihakikishe wanapewa ofisi.
Mbali na hilo, Makonda amemtaka msajili wa vyama vya michezo ahakikishe mpaka Jumatatu katiba ya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) iwe imeshatoka na kukabidhiwa wenyewe.




