Prince Dube aiaga Yanga kwa hisia: Nitawabeba moyoni milele

DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa Zimbabwe, Prince Dube, amewaaga mashabiki wa Yanga, maarufu kama Wananchi, baada ya kutambulishwa rasmi na klabu yake mpya ya Hardrock FC ya Zimbabwe.
Dube amesema ameshindwa hata kupata maneno sahihi ya kuelezea namna anavyoihisi Yanga, akieleza kuwa klabu hiyo imekuwa zaidi ya timu ya mpira wa miguu kwake, bali ni familia iliyompa upendo na imani tangu siku ya kwanza.
“Naona watu walioamini kwangu na kuona mwanga ndani yangu hata pale ambapo sikustahili. Wakati dunia iliona kushindwa, ninyi mliona kitu maalum ndani yangu. Kwa sababu hiyo siioni Yanga kama klabu ya mpira wa miguu pekee, bali ni familia ambayo itakuwa na nafasi ya kipekee moyoni mwangu milele,” amesema Dube.
Mshambuliaji huyo aliwashukuru wadhamini wa klabu, GSM, Rais wa Yanga, Hersi Said, benchi la ufundi, wachezaji wenzake, wafanyakazi wa klabu pamoja na familia yake kwa mchango wao katika kipindi chote alichokitumikia kikosi hicho.
Pia aliwapa shukrani za pekee mashabiki wa Yanga kwa sapoti waliompa kila alipokuwa uwanjani.
“Asante kwa kuifanya safari hii kuwa ya kushangaza. Najinyenyekeza na kusema asanteni sana Wananchi. Shukrani Tanzania, na zaidi ya yote namshukuru Mungu,” alisema.
Dube amejiunga na Hardrock FC baada ya kumaliza safari yake ya kuitumikia Yanga, ambako alikuwa sehemu ya mafanikio ya klabu hiyo katika mashindano ya ndani na kimataifa.




