Ligi Kuu

Pedro: Tuko tayari kuivaa Mbeya City

DAR ES SALAAM: KOCHA mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema kikosi chake kiko imara na tayari kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City, huku akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuondoka na alama tatu kesho.

Akizungumzia mchezo huo Dar es Salaam leo Pedro amesema mchezo wa mwisho ugenini ulikuwa mgumu kutokana na hali ya uwanja, lakini kwa sasa wanaingia kwenye mazingira waliyozoea, jambo linalowapa kujiamini zaidi.

“Kesho tunacheza kwenye mazingira tofauti ambayo tumeyazoea. Nakiri sisi tupo imara zaidi na tunauhitaji mkubwa wa alama tatu. Nafahamu hata wao wanahitaji alama lakini kwetu ni hadithi nyingine,” amesema.

Ameongeza kuwa mabadiliko aliyoyafanya katika mchezo uliopita yalilenga kuwapa nafasi baadhi ya wachezaji kupata utimamu wa mwili pamoja na kupumzisha nyota muhimu, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi katika mchezo ujao.

Kocha huyo amesisitiza umuhimu wa tahadhari wakikabiliana na Mbeya City, akieleza kuwa wapinzani wao wana kikosi chenye uzoefu mkubwa.

“Lazima tuwaheshimu wapinzani wetu. Mbeya City wana kikosi kizuri. Mpira ni mchezo wa makosa, kosa moja linaweza kugharimu matokeo,” ameonya.

Katika upande wa kikosi, Pedro ameeleza kuwa wanatarajia kunufaika na urejeo wa mshambuliaji Prince Dube ambaye alianza kupata dakika chache baada ya kutoka majeruhi, huku akibainisha kuwa bado watamkosa Laurindo Aurelio (Depu) ambaye hajaaanza kurejea uwanjani pamoja na Emanuel Mwanengo.

Kocha huyo amehitimisha kwa kusema wanatarajia mchezo mgumu, lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi na kuwapa burudani mashabiki wao.

Related Articles

Back to top button