Ligi Kuu

Raga yajivunia hatua ya kihistoria Burundi

DAR ES SALAAM: LICHA ya timu ya taifa ya Rugby (raga) kutofanya vizuri kimataifa, Chama cha Rugby Tanzania (TRU) kimesema timu za taifa za wanaume na wanawake katika mashindano ya Burundi Cross-Border Rugby 7s zimeweka historia muhimu katika maendeleo ya mchezo huo nchini.

Mashindano hayo yaliyofanyika jijini Bujumbura yalizikutanisha timu za taifa kutoka Burundi, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Tanzania.

Kwa mara ya kwanza, TRU ilipeleka kwa pamoja timu za taifa za wanaume na wanawake kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa ya raga.

Kwa upande wa wanawake, Tanzania ilipoteza kwa pointi 56-0 dhidi ya Burundi kabla ya kufungwa 58-0 na Uganda. Timu ya wanaume ilianza kwa kupoteza 48-0 dhidi ya Uganda, ikatoka sare ya 0-0 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kisha ikafungwa 55-0 na Burundi.
Katibu Mkuu wa TRU Anthony Dawa, amesema pamoja na matokeo hayo, mashindano yamefikia lengo la kuwapa wachezaji na benchi la ufundi uzoefu muhimu wa kimataifa.

“Mashindano haya yamewapa wachezaji na benchi la ufundi uzoefu mkubwa wa kimataifa. Kushindana na mataifa yenye uzoefu mkubwa wa raga katika ukanda huu kumetuonesha maeneo tunayopaswa kuboresha huku kukichangia maendeleo ya muda mrefu ya mchezo wa raga nchini,” amesema Dawa.

Kwa mujibu wa Dawa, TRU itaendelea kuimarisha timu zake za taifa kwa kuongeza ushiriki katika mashindano ya kimataifa, kuendeleza programu za kukuza vipaji na kuwekeza zaidi katika maendeleo ya timu za wanaume na wanawake kuelekea mashindano yajayo ya kikanda na bara Afrika.

Related Articles

Back to top button