Ligi Kuu

Kipre Junior arejea Azam FC

DAR ES SALAAM: Azam FC imezidi kuonesha dhamira ya kujenga kikosi imara kwa msimu wa 2026/27 baada ya kumrejesha winga wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipré Junior, kutoka MC Alger ya Algeria.

Klabu hiyo ilithibitisha usajili wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii, ikieleza kuwa imemnunua kutoka MC Alger baada ya kuitumikia timu hiyo kwa misimu miwili.

“Tunayo furaha kuwataarifu kuwa tumemrejesha nyota wetu wa zamani Kipré Junior baada ya kumnunua kutoka klabu ya MC Alger. Karibu nyumbani Kipré Junior,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya Azam FC.

Kurejea kwa Kipré kunaleta kumbukumbu tamu kwa mashabiki wa Azam, kwani katika msimu wa 2023/24 aliweka rekodi ya kuvutia kwa kufunga mabao 10 katika mechi 13 za Ligi Kuu ya NBC, akijidhihirisha kuwa mmoja wa wachezaji hatari zaidi wa timu hiyo.

Baada ya kuondoka Azam mwaka 2024, Kipré alijiunga na MC Alger, lakini hakuwa na nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.

Winga huyo anayemudu kucheza pande zote mbili za uwanja anatarajiwa kuongeza kasi na ubunifu katika safu ya ushambuliaji ya Azam FC, huku mashabiki wakiamini kurejea kwake kutairejesha timu hiyo kwenye ushindani mkubwa wa kuwania mataji ya ndani na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button