Kwingineko

Deschamps akiri maumivu ya kipigo, ahoji kiwango cha mwamuzi

TEXAS: Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa, Didier Deschamps, amesema wachezaji wake wameumizwa sana na kipigo cha mabao 2-0 walichopata dhidi ya Hispania katika nusu fainali ya Kombe la Dunia, huku akihoji pia kiwango cha mwamuzi Ivan Barton wa El Salvador.

Akizungumza baada ya mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa AT&T mjini Arlington, Texas, Deschamps amesema Hispania ilikuwa bora zaidi kiufundi na ilistahili ushindi kutokana na namna ilivyodhibiti mchezo.

“Bila shaka kuna maumivu makubwa. Wachezaji wamevunjika moyo kwa sababu tulikuwa na malengo makubwa. Tunapaswa kukubali kuwa tulikuwa chini yao katika ubora wa kiufundi. Lakini kwanza kabisa ni kosa letu, sitaki kumlaumu mtu mwingine,” amesema Deschamps.

Hata hivyo, kocha huyo anayetarajiwa kuondoka baada ya Kombe la Dunia hakuficha kutoridhishwa na maamuzi ya mwamuzi Ivan Barton, hasa baada ya kuipa Hispania penalti kipindi cha kwanza kufuatia Lucas Digne kumchezea vibaya Lamine Yamal ndani ya eneo la hatari.

“Nitawauliza swali lakini sitalijibu. Je, mwamuzi alikuwa na kiwango kinachostahili kuchezesha nusu fainali ya Kombe la Dunia? Sisemi hivyo kwa sababu tumefungwa. Kulikuwa na maamuzi kadhaa yenye utata, ingawa yapo yaliyokuwa kwa faida yetu pia,” amesema Deschamps.

Kwa matokeo hayo, Ufaransa imekosa nafasi ya kucheza fainali na sasa itashuka dimbani kuwania nafasi ya tatu, huku Hispania ikisubiri mshindi wa nusu fainali nyingine kati ya England na Argentina.

Related Articles

Back to top button