Ligi Kuu

Yanga kuingia kambini Julai 20

DAR ES SALAAM: Yanga imeanza kuweka wazi mipango yake kuelekea msimu mpya, ikitangaza ratiba ya maandalizi, mkakati wa usajili, kambi ya timu pamoja na maendeleo ya matibabu ya wachezaji waliokuwa majeruhi.

Akizungumza Dar es Salaam Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga Ally Kamwe amesema shughuli kubwa zinazokuja ni pamoja na Mkutano Mkuu wa wanachama utakaofanyika Agosti 2, ambao pamoja na agenda nyingine utakuwa na uchaguzi wa viongozi.

Uongozi ulieleza kuwa mkutano huo utakuwa tofauti na mikutano iliyopita kutokana na kuhusisha uchaguzi.

Baada ya hapo, Yanga imepanga kufanya utambulisho wa wachezaji wapya na benchi la ufundi, kabla ya kikosi kuripoti kambini Julai 20 kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.

Kambi hiyo itafanyika Avic Town, ambapo uongozi umesema kutokana na muda mfupi uliobaki kabla ya msimu kuanza, hakutakuwa na safari ya maandalizi nje ya nchi.

“Tutakapofungua kambi Avic Town tutafunga milango kwa ajili ya maandalizi maalumu. Hakutakuwa na kuingia na kutoka kiholela, lengo ni kuwapa wachezaji utulivu wa kujiandaa,” amesema.

Kwa upande wa majeruhi, Yanga imesema kipa Khomeini Abubakar ameimarika kwa asilimia 85 baada ya kusumbuliwa na tatizo la nyonga lililomuweka nje kwa muda mrefu. Kipa huyo tayari ameanza kucheza baadhi ya mechi za kirafiki huku akielekea kurejesha kiwango chake cha utimamu wa mwili.

Beki Dickson Job na mshambuliaji Clement Mzize wanaendelea na programu za matibabu na mazoezi ya kurejea uwanjani, huku ripoti za madaktari zikionesha wanaweza kuwa tayari kucheza mechi za ushindani mwishoni mwa Novemba au Desemba.

Kwa upande wa Pacôme Zouzoua, amesema baada ya kufanyiwa upasuaji na kutoka hospitali, anatarajiwa kusafiri kwenda Paris, Ufaransa, kwa ajili ya kuendelea na matibabu na uangalizi maalumu kabla ya kujulikana muda sahihi wa kurejea uwanjani.

Yanga pia inaendelea na maandalizi ya Wiki ya Mwananchi, ambapo uamuzi wa eneo la kufanyika kwa tamasha hilo unatarajiwa kutolewa baada ya kukamilika kwa mazungumzo, huku klabu ikisema licha ya kupata ofa kutoka nje ya nchi, bado inaangalia uwezekano wa kulifanya Tanzania.
Mwisho

Related Articles

Back to top button