“Msimu wa 2024/25 utakuwa wa moto” – Karia

DAR ES SALAAM: RAIS wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF, Wallace Karia amesema msimu wa 2024/25 utakuwa bora zaidi ya uliopita kulingana na mipango yao na maandalizi ya washiriki wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Amesema kwa maandalizi (Pre Season) zilizofanywa na timu zinazoshiriki Ligi Kuu, utakuwa msimu wa ushindani mkubwa kutoka kwa timu zingine mbali na klabu za Simba na Yanga.
Akifungua semina ya waandishi wa habari za michezo kuelekea msimu mpya wa Ligi hiyo inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 16, mwaka huu, Karia amesema anatarajia ukuaji zaidi wa ligi hiyo.
“Msimu wa 2024/25 tunahitaji uwe bora zaidi kuliko msimu uliopita, tumefanikiwa kupunguza na kuongeza kanuni jambo la msimu ni kuwa na ligi bora, ligi sio ya kificho tena, hatutafumbia macho miundo mbinu mibovu au kutaka kuwaridhisha hizi klabu mbili.
Kuwa mmoja akicheza katika uwanja ambao hauna ubora basi na mwingine lazima atumie uwanja huo, tunatamba utakuwa mgumu kulingana na ushindani utakaokuwepo kutika timu zingine,” amesema Karia.
Amesisitiza kuwa kwenye tuzo za msimu wa 2024/25 wataweka kioengele cha tuzo ya chombo cha habari kinachotoa taarifa kwa kuzifikia timu zote bila ya kuangalia Simba na Yanga ambazo zinapewa kipaumbele zaidi.
Karia ameongeza kuwa ligi ya Championship imekuwa na ngumu zaidi ya Ligi zingine ambazo wanazisimamia na kuziendesha kutokana ushindani uliopo kwa timu hizo.